Monday 26 October 2015

SHAIRI


SINA DOGO!

Wapendwa sikilizeni,
Uchoyo si jadi yangu,
Nilosikia jamani,
Mlijue na wenzangu,
Mimi daima napenda,
Kuwajuza wasujua,
Tena hata kuwafunda,
Ili wasije shupaa,
Kwa kujidai vingunge,
Wa habari mitaani,
Na magwiji wa vigenge,
Kwa maneno midomoni,
Haya mwenzenu malenga,
Ngoja niwasimulie,
Ili muupate mwanga,
Elimu mkaitoe,
Ningali ni safarini,
Kigoma kuelekea,
Nimetulia kitini,
Safari kufikiria,
Basi nakuambieni,
Karibu na Ushirombo,
Akaingia chomboni,
Kijana kabeba rambo,
Mrefu mtanashati,
Tabasamu alojaa,
Mwenye kuvalia suti,
Yenye rangi kahawia,
Punde kavunja ukimya,
Kwa kuitoa salamu,
Nikadhani anajipya,
Wengi tusolifahamu,

Wakubwa shikamooni,
Mambo zenu rika langu,
Wadogo nisalimuni,
Marahaba haki yangu,
Baada kusalimia,
Sote tukajituliza,
Hata wenye kusinzia,
Machoni wakajikaza,
Ndiposa yule kijana,
Akaomba usikivu,
Ili apate kunena,
Atujaze uwerevu,
Haikupita dakika,
Abiria kutulia,
Kijana akaridhika,
Pembeni akatulia,
Rambo akalifungua,
Pasi neno kutamka,
Nami nikasubiria,
Kwa shahuku na shufaka,
Punde alipoinuka,
Nami nikanyong’onyea,
Baadhi wakauzika,
Mara walipong’amua,
Kuwa ni muuza dawa,
Auzaye kwenye gari,
Dawa zisokaguliwa,
Ziso kipimo dhahiri,
Basi wengi abiria,
Wakaanza mpuuza,
Kwa kuanza kusinzia,
Huku wakisikiliza,

Naye pasipo kujali,
Bidhaa akazinadi,
Utadhani yu dalali,
Maneno yaso idadi,
Na kwa lugha ya madaha,
Ilosheheni jazanda,
Katu isiyo karaha,
Daima utaipenda,
Kilichotuvunja mbavu,
Dawa ile ya mafua,
Hata walo na uchovu,
Karibu wangezimia,
Vile alivyoeleza,
Si rahisi kutambua,
Japo alisisitiza,
Ingawa hakutoboa,
Alianza kwa kusema,
Chapa simba ndio hii,
Kwa mafua yasokoma,
Hapa lazima ya tii,
Na wenye kipanda uso,
Huyu ndiye mkombozi,
Bwana mwenye utakaso,
Azishindaye hirizi,
Mishipa iliyokaza,
Yenyewe itaachia,
Mgogo ukipakaza,
Wenyewe utaridhia,
Misuli ilolegea,
Imara itasimama,
Mpaka utashangaa,
Vile utakavyolima,

Hata iwe Jumapili,
Kulima utatamani,
Hutaziona dalili,
Za uchovu kiunoni,
Pia naye mtendaji,
Atatenda siku zote,
Hatajali wapitaji,
Huduma sawa kwa wote,
Nanyi mliookoka,
Msipake abadani,
Ili msije potoka,
Mkaasi yenu dini,
Mkalima Jumapili,
Mkaivunja Sabato,
Mkabeza maadili,
Kwa kusingizia joto,
Basi alipomaliza,
Wengi walichekelea,
Dawa wakaimaliza,
Nami sikuambaulia,

No comments:

Post a Comment