Monday 13 October 2014

KIAMBISHI TAMATI "NI"



KIAMBISHI TAMATI “NI”
Makala haya yatashughulikia ufupisho wa makala ya Swahili forum iliyohaririwa na rose – marie beck, Thomas gelder na wemer graefner katika uchambuzi wa kiambishi tamati cha mahali –ni, tathmini na mwisho hitimisho.
Makala haya yanahusu asili na usambaaji wa kiambishi tamati cha mahali –ni. Karibu  lugha zote za kibantu kuna ngeli tatu za mahali zenye viambishi pa, ku, mu, kwa mfano katika lugha ya kisangu viambishi hivi vya mahali  hujitokeza pia katika maneno ya mu-khati, pa-khati, na ku-khati. Kwa upande wa lugha ya kiswahili mofimu hizi yaani pa, ku, mu hutumika kama viwakilishi vionyeshi kwa mfano hapa, huku na humu na vilevile hufanya kazi kama viwakilishi  vimilikishi. Kwa mfano  kwetu, kwao na mwao. Dai hili limetolewa na Beck na wenzake (1994). Swali la msingi, kama viambishi vya mahali vinavyojitokeza katika ngeli hizo, kiambishi –ni- hakipo, kiambishi hiki kimetoka wapi?
Tunapotaka kutaja mahali katika sehemu, hatuwezi kuongeza kiambishi cha mahali pa, mu na ku mwanzoni mwa mzizi katika lugha ya kiswahili kwa mfano neno pori hatuwezi kusema kupori, mupori au papori na badala yake kinawekwa kiambishi tamati cha mahali –ni mwishoni mwa neno kwa mfano porini, ambapo kiambishi –ni kinatumika kuwakilisha ngeli ya 16, 17 na 18. Hata hivyo kuna baadhi ya lugha za kibantu kama Kihehe na Kigogo zinakubali upachikaji huu wa viambishi vya ngeli ya 16, 17 na 18 mwanzoni mwa neno na kuleta maana. Kwa mfano Wahehe wangepachika viambishi hivi katika mzizi wa neno chanya na kuwa pa-chanya, mu-chanya, na ku-chanya.
Kutokana na utata wa kiambishi cha mahali –ni kutoeleweka kimetokea wapi, wataalamu mbalimbali wamejaribu kuelezea asili ya kiambishi –ni. Miongoni mwa wataalamu hao ni pamoja na Claire Gregoire (1975) katika tasnifu yake inayohusu ngeli za mahali katika lugha za kibantu. Anaonesha jinsi kiambishi cha mahali -ni kinavyopatikana katika lugha nyingi za kibantu, huku kikijidhihirisha kama –ini, anatoa mifano ya lugha za kibantu kama  Kikikuyu, kwa mfano jiumba-im, ‘nyumbani’ , Kizulu, kwa mfano ezulwini 'mbinguni' inatokana na neno ‘iizulu’; pia katika lugha ya Kisotho ya Kaskazini tseleng 'njiani' inatokana na neno ‘tsela’; Kichaga mringeny 'majini' inatokana na neno mringa. Kwa hiyo inakubalika kwamba mofimu hii mwanzoni ilikuwa ina umbo la -ini. Ni dhahiri kuwa mofimu hii haijitokeza katika lugha zote za Kibantu.
Carl Meinhof (1942) anatoa bunio lake ambapo anaona kuwa asili ya kiambishi tamati –ni  ni kiwakilishi kionyeshi cha ngeli ya 18 yenye umbo la imwi, umbo hili lilibadilika na kuwa kiambishi mu- na ikalainika wakati wa matumizi na kuwa na umbo m-, ambapo umbo m- likatoweka na kugeuka kiambishi –ni, badiliko hilo limetokea katika mofimu ya nafsi ya pili wingi ambayo ni mu kama kiambishi cha kitenzi lakini inaonekana kama nyi au ni ikitumiwa kama kiwakilishi cha nafsi yaani ninyi.
Kwa hakika Meinof ameshindwa kuonesha kiambishi –ni kwa uangavu wake, kwani anakihusisha tena na kiambishi cha nafsi wakati mjadala ni kiambishi –ni kama kiambishi cha mahali. Ingawa anatuonesha utokezaji huo wa –ni kama –nyi, dai hili linajidhihirisha pia katika baadhi ya lugha za Kibantu pale kiambishi –ni kinapojitokeza kama –nyi, tuchunguze data ifuatayo: Katika lugha ya Kigweno viambishi tamati vya mahali vinawakilishwa na –nyi kwa mfano mghundenyi - shambani, mtonyi - mtoni, mreminyi - migombani, kwa mantiki hiyo kiambishi tamati –nyi ni kiwakilishi kionyeshi cha ngeli ya 18 katika lugha ya kigweno lakini baadhi ya lugha za kibantu zinakataa mchakato wa upachikaji wa kiambishi –nyi, kiswahili kikiwa kimojawapo. Hata hivyo dhana ya meinhof si ngeni kwani tayari ilishashughulikiwa na Raum (1909) katika sarufi ya Kichaga.
Vilevile Charles Sacleux (1939) anatoa nadharia tete tofauti juu ya asili ya kiambishi tamati –ni. Kwa mtazamo wake anaona kiambishi tamati –ni kimetokana na neno ini, pamoja na maoni yake haoneshi zaidi uhusiano wa kiambishi tamati –ni na neno ini ila katika lahaja ya Kiteita watu husema nyumbeni yaani nyumba na ini.  Mabadiliko ya  kupanda na kushuka kwa toni katika neno nyumbeni hukasabisha kutokea kwa nyumba na ini. Hata hivyo dai hili halikushughulikiwa na wataalamu wengine kuhusu mabadiliko ya neno –ini na kuwa kiambishi –ni.
Wataalam mbalimbali kama Nabhany anajaribu kutoa maana ya neno ini kwa kuielekeza fikra hiyo kuwa kiambishi tamati –ini kinatokana na jina ini lenye maana ya 'kinofu chekundu cha ndani ya mwili kilichojaa damu na kinachotoa nyongo kusaidia kuyeyusha chakula tumboni'.
Kutokana na dhana hiyo, Marie na wenzake wanadai kuwa katika Kiswahili maana na matumizi ya neno ini ni kiungo cha ndani ya mwili wa binadamu na katika mnyambuliko wa jina, ini katika ngeli ya 7 ni kiini, hivyo kiambishi tamati –ni ni kiini cha kiambishi tamati cha mahali. Katika baadhi ya lahaja za kiswahili kama Kimvita inaonyesha kiambishi tamati cha mahali –ni ni ngeli ya 18.
Hivyo wanaendelea kudai kuwa kiambishi cha mahali –ni kimesambaa kutoka lugha moja na kwenda lugha nyingine, na lugha hiyo ni kiswahili. Wanaeleza kuwa Kiswahili kilikuwa na kiambishi -ni toka zamani. Kuna miji inayothibitisha hilo, miji hiyo ni Quelimani (Kilimani) huko msumbiji na moroni (Motoni) katika visiwa vya Komoro, baadaye kiambishi hiki kilienea katika baadhi ya lugha za kibantu kama Kikuyu, Kisambaa na lugha za Kisabiki.
Pendekezo hili lina udhaifu kwani ukubwa wa eneo la kiambishi tamati –ni, umeenea sehemu kubwa hasa sehemu ambazo waswahili walipita kwa mfano Afrika ya Kusini, Msumbiji ya kati na visiwa vya Komoro. Hata hivyo hatuna ushahidi wa kueleza hawa watu walisafiri vipi na lengo la safari yao ilikuwa ni nini?  Hata maneno ya Kiswahili yanayofanana na baadhi ya makabila ya Afrika Kusini, Msumbiji na Visiwa vya Comoro ni kwa sababu Kiswahili ni Kibantu hivyo kuna baadhi ya misamiati inaingiliana na lugha ya kiswahili.
Pamoja na nadharia tete mbalimbali za hapo juu na dhana mbalimbali zilizojengwa na wataalam mbalimbali kuhusu mofimu ya mahali –ni, kuna baadhi ya madai yao yanaonekana kuwa na nguvu na pia kuna udhaifu unaojidhihirisha:
Mtazamo wa  Raum-Meinhof una udhaifu wake katika utafutaji wa chimbuko la  kiambishi –ni kwa kusisitiza kwamba kiwakilishi cha mahali cha Kiherero imwi 'humu', ambacho alifikiri kwamba ni asili ya -(i)ni, hakijulikani katika maenezi yake. Kanuni ya kubadilisha imwi kuwa ini si wazi kabisa.
Kama tunakubaliana na Charles Sacleux kwa madai yake ya asili ya kiambishi tamati cha mahali –ni ni ini ya mahali inatulazimu tuthibitishe uwezekano wa kubadirika kwa neno ini na kuwa kiambishi –ni. Hata hivyo hakuna uthibitisho wa  asili ya kiambishi –ni ni ini kwasababu hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha mchakato wa neno ini kuwa kiambishi –ni.
Hata hivyo kuna ukweli wa kiambishi –ni kufungamana na ngeli za mahali kwa sababu baadhi ya nomino haziwezi kuwakilishwa na viambishi vya mahali vya ngeli ya 16, 17 na 18 na badala yake kiambishi tamati cha mahali –ni kimewakilisha ngeli hizo.
Kwani nini mofimu –ni ihusishwe na lugha ya Kiswahili, pamoja na sababu mbalimbali zilizotolewa na wataalam mbalimbali, pia inaonekana katika lugha mbalimbali za Kibantu kama zilivyojidhihirisha hapo juu, mofimu –ni inajitokeza katika sura mbalimbali. Hivyo ni vigumu kuinasibisha na lugha hizo za Kibantu tofauti na Kiswahili, ambacho inachukua sura ya aina moja, yaani –ni na kujitokeza mwishoni mwa nomino.
 Kwa kuhitimisha tunasema kiambishi cha mahali –ni kina utata katika utokeaji na usambaaji wake hivyo tafiti nyingi zinatakiwa ili kujua chanzo cha kiambishi cha mahali –ni.

No comments:

Post a Comment