Wednesday 27 November 2013

UTENDI WA SON-JARA


UTENDI WA SON- JARA
Dhana ya utendi katika fasihi ya Kiswahili, iliwahi kuzua utata baada ya Ruth Finnegan (1970) kusema kwamba Afrika hakuna tendi bali kuna simulizi za kisifo. Hoja hii aliipa uzito kutokana kwamba aliangalia tendi andishi na kusahau tendi simulizi. Vilevile vipengele muhimu vya tendi simulizi hakuvipa umuhimu kama vile usimulizi na utendaji. Vigezo muhimu alivyovitaja ni :
(1)Utendi uwe na umbo la kinudhumu.
(2)Urefu.
(3)Uzungumzie maisha ya shujaa.
(4)Muunganiko wa matukio.
Kutokana na vigezo hivyo aliona kwamba kuna tendi zenye sifa hizo, isipokuwa sifa ya nudhumu na tendi hizo ni Son-Jara, Mwendo na Lianja. Madai yake yaliibua wataalamu mbalimbali kufatiti na...
kuandika kuhusu tendi, baadhi yao ni Okpewho (1979),Mbele(1977), Mulokozi (1987) ambao wameangalia utendi wa kiafrika kama utendi simulizi tofauti na ilivyo kwa Finnegan. (Mulokozi 2002: 2-5) Baada ya tafiti hizo ilionekana kwamba Afrika kuna tendi.

Mulokozi (1996:85) anasema utendi ni utanzu mashuhuri sana katika kundi la ghani-simulizi. Anaendelea kusema kuwa utendi ni ushairi wa matendo. Ni utungo mrefu wenye kusimulia matukio ya kishujaa yenye uzito wa kijamii au kitaifa. Matukio haya huweza kuwa ya kihistoria na visakale/visasili.
Naye mtaalamu Bowra (1952) anatumia fomula kuelezea maana ya utendi kwa lugha ya Kiingereza. Anasema E = M + Ms (Epic = Mars + Muse/Music), ikiwa na maana kwamba utendi ni vita na muziki (u = m + v).
Kwa upande wa Wamitila (2003:333) anafasili utendi kuwa ni shairi refu la kisimulizi linalozungumzia kwa mapana na mtindo wa hali ya juu matendo ya mashujaa au shujaa mmoja. Kimsingi utendi huwa na sifa nyingi na huweza kuleta pamoja hadithi ya kishujaa, mugani, visasili.
Hivyo tunaweza kufasili utendi kuwa ni utungo mrefu wa kishairi wenye kusimulia matukio ya kishujaa au ya kihistoria. Vilevile utendi unaweza kuwa umebeba au unasimulia historia ya jamii fulani kwa sababu unaweza kuelezea mashujaa waliopata kuishi na matendo yao. Hivyo utendi unaweza kuhusu asili ya jamii fulani na vilevile unaweza kuhusu maisha ya shujaa na mapambano anayopitia.
UTANGULIZI
John William Johnson ni mtafiti na mfasiri wa utendi wa Son-Jara.Alifanya utafiti wake kwenye miaka ya 70 na kuchapishwa mwaka 1986 na Library Congress Cataloging in Publication Data.
Mwimbaji wa utendi ni Jeli Fa-Digi Sisoko alikuwa na wake wane.Alikuwa mwimbaji na mshairi, mtoto wake wa kiume aliyeitwa Magan Sisoko naye alikuwa mwimbaji wa tendi.Jina la Magan limejitokeza katika tendi kama jina mojawapo la Baba yake Son-Jara.Kwa mujibu wa mtafiti wa utendi huu Magan mtoto wa Magan Sisoko ndiye aliyempa historia kuhusu utendi kwa ujumla na alimweleza kuhusu maisha ya Baba yake. Ingawa kisa ya Son-Jara kinasimuliwa kwa muundo wa utendi, wapo waandishi ambao wametumia ubunifu wao katika kusimulia kisa cha Son-Jara katika muundo wa Riwaya na Tamthilia.
 Mbogo, E kutokana na kisa cha Son-Jara ameandika tamthilia yenye muundo wa Ki-Aristotle ambapo mashujaa wanaishia na anguko. Niane, D.T ameandika katika muundo wa riwaya na kilichapwa kwa mara ya kwanza 1965. Kutokana na kisa cha Sundiata na waandishi tofauti, majina na wahusika yametumika tofauti kulingana na lugha waliyotafsiria au waliyoandikia mfano adui wa Son–jara waandishi wamemwita Sumanguru au Soumaoro na Sumanguru.
USULI WA SUNDIATA (SON-JARA) KAMA SHUJAA.
Sundiata ni shujaa wa kiutamaduni wa makabila mengi ya Afrika Magharibi hasa yale yenye kuzungumza lugha ya Kimande: Wa-Bambara, Wa-Khasonke, Wa-Susu, Wa-Jula, Wa-Wangara, Wa-Wasoninke, Wa-Mandinka na Wa-mandenka. Wanahistoria wanamchukulia kwamba ni mwanzilishi wa himaya ya Mali, na mmoja wa viongozi mashughuli aliyepanda na kushuka katika himaya ya pana ya magharibi ya Sudan katika zama za kale. Hivyo ni binadamu wa kihistoria. Ushujaa wake unazungumziwa katika katika tendi na hadithi mbalimbali zinazohusu historia, mila za jamii na mambo ya kiutawala.
USULI WA UTENDI.
Utendi wa Son-Jara ni utendi wa kihistoria unaohusu maisha ya Son-Jara kabla ya kuzaliwa, wakati wa kuzaliwa na matukio yaliyompata na ushujaa wake. Baba yake, Fatta Magan alikuwa mtawala wa nchi ya Manden (Mali).Baba yake alitabiriwa kwamba atamuoa mwanamke mwanamke wa pili mwenye sura mbaya aitwaye Sugulun Konde. Naye atamzalia mtoto wa kiume ambaye atakuwa mtawala mrithi wake (ubeti 998-1005).Baada ya fatta –Magan kumuoa Sugulun Konde, wake zake wote walipata ujauzito na walijifungua siku moja.
Mke wa kwanza, Saman Berete alipojifungua mwanamke mzee alitumwa kwenda kumuambia Fatta-Magan ambaye alikuwa mji mwingine, kuwa mke wake amejifungua mtoto wa kiume. Alipofika alikuta watu wanakula, alipokaribishwa alianza kula na kusahau kutoa. Lakini Sugulun alipojifungua alitumwa mshairi Tumu Maniya, ambapo alipofika kwa Mfalme alikaribishwa kula lakini alikataa kula kwa madai kwamba mpaka atoe ujumbe wake aliopewa. Baada ya kutoa taarifa yule mwanamke wa kwanza akaeleza kuwa naye alikuwa na taarifa kama hiyo. Hata hivyo Mfalme alimtambua Son-Jara, mtoto wa Sugulun kuwa ndiye mzaliwa wa kwanza na atakuwa mrithi wake. Taarifa hizo zilipomfikia Saman Berete kuwa mwanaye Dankaran Tuman hakutambuliwa kama mzaliwa wa kwanza aliomba kwa miungu hali iliyosababisha Son-Jara asitembee kwa muda wa miaka tisa.
Kutokana na utabiri wa jinn kuhusu kutembea kwa Son-Jara na pia kuna kafara zilizofanyika (ubeti 1260-1535) kafara hiyo ilifanywa kwenye mti wa mbuyu ambao wanawake wa Manden walitumia majani yake kutengenezea supu.Hivyo ilisababisha Son-Jara kupata nguvu ya kuuung,a mbuyu huo na kwenda kuupanda kando ya nyumba ya mama yake.Na huo ndio mwanzo wa kutembea kwa Son-Jara  na ushujaa wake kuonekana kuonekana hata alipokwenda msituni kuwinda.
Baada ya Fatta-Magan kufariki Dankaran Tuman na mama yake walitumia uchawi ili Dankaran awe mrithi wa Baba yake. Hali iliyoleta mgogoro na kusababisha Son-Jara na mama yake kuondoka Manden na kwenda kukaa uhamishoni Mema kwa muda wa miaka saba.Wakati Son-Jara akiwa bado uhamishoni,shujaa Sumamuru alipambana na Dankaran aliyeshika madaraka na kumshinda na kusababisha Sumamuru kutawala himaya ya Manden.Baadaye Son-Jara alipata hizo taarifa aliamua kurudi Manden na kupambana na Sumamuru ila alishindwa (ubeti 2635).Kushindwa kwa Son-Jara kulisababisha dada yake Sugulun Kulunkan aliamua kumsaidia kaka yake kwa kutumia hila ya kuolewa na Sumanguru ili ajue siri ya nguvu ya Sumanguru. Matokeo ya hila hiyo ni kufanikiwa kujua siri ambayo alimpa kaka yake na kumwezesha kumshinda adui yake.
Mtafiti Johnson katika utafiti wa utendi huu aligawa sifa za tendi katika makundi mawili yaani sifa za kimuundo na sifa za kimuktadha.Katika sifa za kimuundo kuna vipengele vifuatavyo:
1. Utendi ni ushairi.
Sifa hii imejitokeza katika utendi wa Son-Jara kwani uko umbo la kishairi, kuna upangilifu wa beti 3080. Ni utendi unaotumia muziki kutokana na vifaa vinavyotajwa kama kora.Vile vile kuna dhana kujirudiarudia kwa mistari (ubeti 2470)
 2. Usimulizi.
Utendi huu una masimulizi ya uumbaji wa Mungu kwa Adamu na Eva. Vile vile una majibizano ya Mungu na ibilisi (ubeti 50-75)
  • Una kisa cha zamani cha Kala Jula Sangoyi mshairi wa Manden.Pia kuna uitikiaji ambao  unajitokeza katika fasihi simulizi.Mfano ndio ,ukweli n.k
  • Usimulizi huu pia umeambatana na nyimbo mbali mbali kutokana na matukio tofauti.
 3. Ushujaa.
Utendi huwa unahusu ushujaa. Ushujaa wa Son-Jara, Sumamuru na mwanamke wa Nyati.
 4. Visakale.
Utendi una visakale vya Biblia mfano kuhusu uumbaji wa Mungu, majibizano ya Mungu na Adamu n.k
5. Urefu.
Hiki ni kipengele kilichopendekezwa pia na Ruth Finnegan, utendi huu ni mrefu wenye beti 3080. Pamoja na kuelezea maisha ya Son-Jara kabla ya kuzaliwa, baada ya kuzaliwa na vikwazo alivyopitia hadi kutawala kwake, tunaelezwa pia visa vya biblia hasa kuhusu uumbaji wa Adamu na Eva na asili ya koo mbalimbali.
6. Uamilifu mwingi.
Utendi huu una mambo mengi ambayo yako kwenye jamii mfano ngano, visasili na nyimbo.
Simulizi za kimuktadha.
  • Utendi unahusu mambo mengi 
  • Una vita 
  •  Asili ya koo mbalimbali 
  • Mila na desturi za jamii ya Mande mfano masuala ya matambiko, salamu na vyakula. 
  • Kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Hii imejitokeza ndio maana utendi huu umesimuliwa katika mataifa mbalimbali.Utendi wa Son-Jara umepatikana katika nchi za Ghana, Sudan, Gambia, Ivory Coast, Mali, na Mauritius.
MAUDHUI.
Maudhui ya utendi huu yamejengwa kupitia mgogoro unaohusu utawala wa himaya ya Mali ambapo mwanzoni kakake Son-Jara, Dankaran Tuman ambaye walifanya hila na mama yake ili atawale himaya ya Manden (Mali).Hali hii ilisababisha Son-Jara kuhama Manden na kwenda kuishi Mema na mama yake.Vile vile kuna mgogoro mwingine kati ya Son-Jara na Sumamuru uliohusu ardhi ya Manden.Mwanzoni tunaelezwa kuwa Son-Jara alikuwa anashindwa lakini baadaye alimshinda adui yake.
DHAMIRA NDOGONDOGO.
Mila na Desturi.
Taratibu za mila na desturi za Waafrika kijana wa kiume mdogo au binti wa kike mdogo hatakiwi kuoa au kuolewa kabla ya mkubwa wake kuoa au kuolewa.Hii imejitokeza kwa kaka mkubwa ambaye ni Dan Mansa Wulanba na mdogo wake ni Dan Mansa Wulandin (950-61).
Kwenye suala la salamu,mila na desturi ya Wa-Manden kuna salamu ya wanaume wanaamkia” ilu tuntun” wanaitikia” tuntun bere “  wanawake wanasalimia” ilu konkon” wanajibu” konkon logoso “
Mila na utamaduni; mama yake Son-Jara aliona kuwa kitendo cha mtoto wake kutotembea sio kwamba alilala na mwanaume mwingine. (1395-1400).Hivyo anaapa kudhihirisha kwamba ni mume huyo huyo mmoja aliyelala naye.
Wivu.
Dhamira hii imejengwa kwa kutumia mke wa kwanza wa Fatta Magan.Wivu huu ulitokana na utabiri wa Son-Jara aliyeonekana kuwa ndio atakuwa mtawala wa Manden.Berete aliomba kwa Mungu ili Son-Jara asitembee (ubeti 1150).Wivu wake ndio chanzo cha mgogoro uliosababisha Son-Jara na mama yake kwenda Mema.Uamuzi wao kuondoka umejengwa kupitia maneno yanayosema; “Kukaa hakutatui tatizo Kusafiri kunatatua tatizo.” (hiyo ni kweli) Maneno hayo yanasaidia kujenga motifu ya msako.
Mapenzi.
Mapenzi kati ya Son-Jara na mama yake.Mama yake So-Jara anaonesha mapenzi kwa mtoto  wake, hali iliyomfanya ahangaike kwa kumlilia Mungu.Mapenzi kati ya Son-Jara na dada yake pale ambapo Sugulun aliamua kukubali kuolewa na Sumamuru ili aweze kujua siri ya ushujaa wake.Sumamuru nguvu zake zilikuwa kwenye nyumba yake.
Uchu wa madaraka.
Dhana hii imejengwa kupitia Dankaran Tuman akishirikiana na mama yake ambapo walitumia mbinu ya uchawi ili kupata madaraka ambayo Son-Jara ndiye aliyetakiwa kuyapata.Pia dhana ya madaraka imejengwa kupitia mhusika Sumamuru ambaye aliuangusha utawala wa Dankaran na kutawala yeye.
DHANA YA MOTIFU
Son-Jara kusafiri kutoka Manden kwenda Mema.Motifu hii ilimsaidia kujiimarisha kinguvu.Pia inaendana na sifa ya shujaa wa Kimande ambaye hutakiwa atoke katika jamii yake ili apambane na vikwazo ambapo anapovishinda vinamjengea nguvu ya kuwa shujaa. Pia mashujaa wa Mande kulingana na utamaduni wao hawana budi wawe na uwezo wa kutumia nguvu (zilizofichika) za sihiri ili kuwafikisha kwenye makusudio yao.Mfano wa vikwazo vilivyojitokeza ni:-
Pale Mfalme Mansa Konkon alipomkaribisha Son-Jara kucheza mchezo wa ushindi, na kama angeshindwa angeuawa.Matokeo yake Son-Jara alishinda, kitendo kilichomfanya afukuzwe Djedeba.
Son-jara na mama yake walipokuwa katika mji wa Mema, Son-Jara alipigana vita vilivyoonesha ushujaa wake, jambo lililomfanya aheshimike kwa Mfalme.Hata hivyo alipata kikwazo kingine pale alipotaka kurudi Manden na kabla ya kuondoka mama yake alifariki .Son-jara aliomba amzike mama yake ila Mfalme alikataa na alimwambia kama anataka aIipie ardhi.Hivyo alikubali, lakini alileta mkoba wenye vitu mbalimbali kama manyoya ya kuku, ”pot shells” na mabua. Baada ya Mfalme kuviona vitu hivyo alikasirika na kutaka kumwadhibu, hata hivyo msaidizi wake akamwambia kuwa vitu hivyo vinaashiria uharibifu na asipomruhusu kumzika mama yake mambo mabaya yatatokea. Mfalme alikubali kumpa Son-Jara ardhi ya kumzika mama yake.
Motifu ya msako.
Hii imejitokeza pale ambapo Son-Jara alipokuwa Mema, watu wa Manden walipompelekea taarifa kuwa kulikuwa na uongozi mbaya wa Sumamuru. Hivyo alirudi Manden ili kupambana na Sumamuru kwa ajili ya kupata uongozi.
Motifu ya safari na motifu ya msako, pia zimejenga ruwaza ya shujaa, ambapo kwa mujibu wa Campbell (1956) shujaa ana hatua tatu za ruwaza:
  • Hatua ya kuondoka shujaa. 
  • Kukutana na vikwazo na kuvishinda. 
  • Kurudi katika jamii na kupigana na kupata ushindi.
Shujaa Son-Jara alipitia hatua zote hizo tatu,yaani aliondoka Manden akaenda Mema, akakutana na vikwazo na kuvishinda kasha akarudi Manden.
FANI.
Wahusika.
Son-Jara
Huyu ndiye shujaa wa kihistoria na utendi huu umejengwa juu yake.Mawazo ya wataalamu mbalimbali yanasema kwamba shujaa wa Ki-mande anaongozwa na nguvu za ba-denya na fa-denya.Fa-denya ni kani ya kiume.Son-Jara alipata nguvu hizo kutoka kwa Baba yake.Tunaoneshwa kuwa Baba yake alikuwa mkimbizi kutoka Mecca.Hivyo Son-Jara alipata barakah.Ba-denya ni kani ya kike na Son-Jara aliipata nguvu hiyo iliitwa nyama kutoka kwa mama yake ambaye alikuwa binti wa mwanamke wa Nyati (The Buffalo woman).Hizi nguvu mbili ndizo zinazomwezesha shujaa kupata nguvu ya ushindi. Kuna hoja kwamba huenda Son-Jara mwanzoni alikuwa anashindwa na Sumamuru kwa sababu mama yake alishafariki. Vilevile huenda kuna ukweli kwani Sugulun dada yake ndiye aliyemsaidia kupata nguvu ya kumshinda adui yake.
Shujaa wa Ki-Mande lazima awe na wasaidizi. Son-Jara alikuwa na msaidizi Balla Fasseke (mshairi) ambaye alitoroka kwa Susu Sumamuru na akajiunga kwenye kambi ya Son-Jara. Msaidizi mwingine ni Fa-Koli (binamu yake Sumamuru) lakini alimtoroka na kwenda kujiunga na Son-Jara.Wasaidizi wengine ni pamoja na washairi na waganga.
Shujaa wa Ki-Mande anakuwa na kinga ambayo lazima adui yake ajue ilipo: Siri hiyo ilifichuliwa na dada yake Son-Jara kuhusu Sumamuru. Hii pia inafanana na utendi wa Rukiza ambapo mtoto wa Rukiza ndiye aliyetoa siri ya ushujaa wa Baba yake.
Shujaa anazaliwa na mwanamke bikira: Son-Jara amezaliwa na mwanamke bikira aliye na sura mbaya (Sugulun Konde).
Son-Jara amepewa jina hilo kutokana na mila na desturi za jamii ya Mali, ambapo jina la shujaa hutokana na viambishi awali vya jina la mama yake. Sugulun ni suun ambapo tunapata jina la Sundiata na Sogolon ni soon ambapo tunapata jina la Son-Jara. Pia alipewa majina mbalimbali ya kishujaa yenye kubeba maana kama vile: Nare Magan Konate; Nare ni jina la sehemu mojawapo katika mji wa Mali, na watu huamini kuwa ilikuwa himaya ya Son-Jara. Magan ni jina alilopewa Son- Jara likiwa na maana ya mwanamume mwenye nguvu.Majina mengine ni:
1.   Msababishi wa hasara (causer of loss) .Hii inaonesha ukatili wake.
2.   Mkuki wa hasira, Mkuki wa huduma ikiwa na mana ya nguvu za kuonesha ushujaa.
3.   Mungu wa vita (Warlord ) Hii inasisitiza ukatili.
4.   Mtemi Simba (Lion -chief) ikiwa inaonesha ukuu, nguvu na utawala.
Sumamuru:
Huyu ni shujaa aliyepambana na Son-Jara, na anatumia nguvu za sihiri ili kuweza kumshinda adui. Alikuwa anapenda kuchukua wake za watu, mfano alimchukua mke wa binamu yake Fa-Koli. Alikuwa kiongozi dhalimu kwani aliwatoza watu kodi kubwa, jambo lililochangia kumtafuta Son-Jara ili aje atawale. Alipambana na Son-Jara kwa mara ya kwanza na kumshinda, akapambana na Dankaran na kumshinda mwisho akatawala Manden. Vilevile alipambana na Son-Jara kwa mara ya pili na kushindwa. Hivyo ilimfanya kutotawala tena Manden.
Suguluni Konde.
Ni mama yake Son-Jara, alijulikana pia kwa jina la mama wa mchawi. Ni mama aliyeishi kwa huzuni kubwa mwanzoni kwani mtoto wake alikuwa kilema, hali iliyomfanya asikubalike katika jamii. Kwa mfano wanawake wenzake walikataa kumpa majani ya mbuyu kwa ajili ya kutengeneza supu, ambapo majani hayo yalitakiwa kuchumwa na watoto wa kiume. Walimtolea maneno ya kashfa wakisema:
“Nenda ukamwambie huyo mtoto wako kilema
Akuchumie ya kwako.
Haya nimechumiwa na mtoto wangu.”(1299-1301)
Hata hivyo hali ilibadilika pale Son-Jara alipoweza kusimama na kutembea.Alilipiza kisasi kwa kung’oa mbuyu na kumpelekea mama yake nyumbani, ambapo aliupanda na kumwambia mama yake kuwa wanawake watakuja kuchuma majani kwake.Tukio hili lilimwondolea mama yake kejeli na dharau alizokuwa anazipata. 
Kwa mujibu wa Lord Raglan (1934) mama wa shujaa anatakiwa awe bikira. Suguluni alikuwa bikira lakini mwanamke mwenye sura mbaya. Utabiri wa Suguluni kuolewa  na kuzaa mtoto na Fata Magan uliishatabiriwa.Hii inafananishwa na kuzaliwa kwa Yesu ambapo kulikuwa na utabiri wa mama yake (Bikira Maria ).
Lugha.
Lugha iliyotumika ni ya kishairi pamoja na kwamba imetafsiriwa katika lugha ya kiingereza, imejaa misemo, lugha ya picha, methali na tamathali za semi.
Tamathali za semi.
Sitiari.
Taraweres,
“Mimi ni nyati wa nchi ya Du”.hii inaonesha jinsi mwanamke huyu alivyofananishwa na nyati, na pia inabeba dhana ya majigambo.
Tafsida.”kutafuta burudani na wajibu kwa mkewe.’ (ubeti 968) Hii ni lugha inayotokana na sharia za kiislamu kwamba mwanamume kufanya tendo la ndoa na mkewe ni wajibu na humburudisha.
Lugha ya picha:
(2021 -22) Maziwa ya Ijumaa (Friday milk) kutokana na jamii ya Manden ndio yanayofaa kwa tambiko. Son Jara alimwambia sumamuru kwamba hawezi kuongoza Manden kwa sababu yeye hastahili kuongoza.
“Waambie safari ya nchi ya Du imekuwa nzuri.” (1066) Hii ilikuwa ina maana kwamba mwanamke Sugulum Konde amepata ujauzito, pia hii inadhihirisha ontolojia ya kiafrika kuwa baada ya ndoa ni  lazima familia ipate mtoto.
Picha na Ishara
(ubeti 873-76) Paka aliyepita kwenye miguu ya Sugulun aliyokuwa ameibana iliashiria uwezo wa kufanya tendo la ndoa na kuzaa. Suala la mwanamke kukaa na kubana miguu linajenga pia dhana ya mila na desturi za Kiafrika.
Majigambo:
Haya yamejitokeza pale mwanamke wa Nyati alipokuwa akijigamba mbele ya wawindaji wawili (Dan Mansa Wulanba, Dan Mansa wulandin)
“Hakuna bunduki inayoweza kunitoboaHakuna mkuki unaoweza kunitoboa
Hakuna kisu kinachoweza kunitoboa.” (ubeti 620)
Aliyejigamba ni mke wa Nyati kuhusu nguvu zake. Majigambo ya mwanamke wa Nyati mbele ya Tarawere. Hii inaonesha sifa ya shujaa kuwa ana nguvu.
Fomula:
Fomula imetumika simulizi
 Paka alizunguka na kuzunguruka
Paka alizunguruka na kuzunguruka
Paka alipita katikati ya miguu ya Konde(ubeti 917)
Hii inafafanua jinsi paka alivyotumika kiishara alipopita katikati ya miguu ya Maiden.
Muundo
Kimeanza moja kwa moja sawa na muundo wa kitabnu cha mwanzo katika Biblia. Unaendelea kuelezea muktadha wa mbinguni katika uumbaji wa Adamu na Eva na inaelezea nasaba ya kiislamu na familia za maude Mpaka familia ya Babake Son-Jara. (-260) ambapo alianzisha ukoo wenye hadhi ya juu.
Mtindo: Mtunzi ametumia Mbinu mbalimbali mfano mbinu ya unyume.
Na pale watakapokwenda Msituni kifaru ataenda mjini
        Na pale watakaporudi mjini kifaru atakwenda msituni (ubeti 530)
Viitikio vya washairi
Ni kweli, kweli, Mmh. Hivi ni viitikio  vilivyokuwa vinatumiwa  kutokana na wazo linalotolewa.
“Kusafiri kunatatua tatizo                           ( kweli)
Walikwenda                                                (Ni kweli)
Walifika kwenye msitu mnene”                  ( Mmm)
Hapa tunapata motifu ya safari ambayo inaashiria kulikuwa na mapambano.
Mbinu ya kutumia namba: Mfano namba tatu inajitokeza katika suala la uzazi.Noah alikuwa na watoto 3 wa kiume ambao ni Ham, Shem na Japhet. Bilali alikuwa na wajukuu watatu, Kanu Simbon, Kanu Nyogon Simbon na Lawali Simbon. (uk.104-105) Namba tatu Kibiblia inamaanisha utatu mtakatifu, yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.
Namba 7 imejitokeza pale Jini alipowaambia wakina Dan Mansa Wulandin ili awafanyie mazingaombwe, wanatakiwa kutoa mbuzi saba kwa ajili ya kafara na ndipo watapata siri ya nguvu za mwanamke wa Nyati (Buffalo Woman). Katika imani ya Kiislamu namba saba ina-maanisha mbingu saba, na upande wa Wakristu ina maana ya siku saba za uumbaji wa Mungu.
Mbinu ya kicheko: Mbinu hii ya kicheko inaashiria dharau aliyokuwa mwanamke wa Nyati kwa Wa- Tarawere. Mwanamke wa Nyati alisema: “Ha! Ninyi ni wakina nani?” (uk. 115)
Mandhari
Mandhari ya utendi ni pana kwa sababu imehusisha nchi mbalimbali za Afrika. Lakini matukio yamejitokeza katika nchi ya Mema, Manden na Du. Mandhari hizo zina taswira ya tamaduni nyingi za nchi za Afrika hasa katika suala la viapo, matambiko, kafara, salamu za wanawake na wanaume na sifa za mashujaa.
Hitimisho
Utendi huu una sifa bainifu ambazo zina ufanano na tendi za Afrika Mashariki mfano mbinu ya usimulizi, suala la dadake Son-Jara kuolewa na Sumamuru ni sawa na utendi wa Rukiza ambapo binti ya Rukiza aliolewa na Ruhinda. Mti wa Mbuyu unatumika katika matambiko ya Afrika Mashariki.Utendi wa Son-Jara una mambo mbalimbali yanayohusu kuanzishwa kwa himaya ya Mali, Visa vya kwenye Biblia, Mila na desturi za waafrika, Hivyo unatoa mafunzo mbali mbali kwa jamii.
Kufanana kwa utendi wa Son – Jara na tendi nyingine.
-Nguvu zilizo nje ya uwezo wa mwanadamu: Liyongo aliweza kubeba mkoba ulikuwa na vitu vilivyoweza kujaza nyumba nzima. Kwa upande wa Son-Jara siku aliyoweza kuondokana na kilema chake, aliweza kuung’oa mti wa mbuyu na kuupanda nyumbani kwa mama yake.
-Ni ngano inayosimulia maisha ya Liyongo na ile inayosimulia maisha ya Son-Jara zina mambo ya kishujaa yanayohusiana na jamii husika ambayo yametiliwa chumvi ili kumjenga shujaa wa kihistoria.
-Tendi hizi zina dhana ya wivu wa kindugu katika suala la madaraka.Katika utendi wa Son-Jara, kaka yake, Dankaran Tuman alimuonea wivu Son-Jara hali iliyosababisha Son-Jara na mama yake wahamie Mema. Kwa upande wa Liyongo, kaka yake alimuonea wivu na kutafuta mbinu mbalimbali za kumuua mpaka akafanikiwa.
MAREJEO.
Innes, G (1974) Sunjata three Mandika versions, London, University of London.
Johnson, J.W (1986), THE EPIC OF SON-JARA-A West African Tradition, Analytical Study and Translation,Bloomington: Indiana University Press.
Mbogo, E ( 1994) Sundiata, Kisumu: Lake Publishers and Enterprises Ltd.
Mulokozi, M. (1996) Fasihi ya Kiswahili: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Mulokozi, M.M. (2002) The African Epic Controversy: Historical, Philosophical and Aesthetic perspectives on Epics Poetry and performance, Dar es Salaam: Mkuki na Nyota.
Niane, D. T (1965) Sundiata:An Epic of Old Mali, Longmans,Green and Co.Ltd.
Wamitila K.W (2003) Kamusi ya Fasihi Istilahi na Nadharia: Focus Publication Ltd.

No comments:

Post a Comment