Friday 1 November 2013

SANAA ZA MAONESHO



SANAA ZA MAONESHO KABLA YA UKOLONI AFRIKA MASHARIKI NA MBINU ZILIZOTUMIKA KUFIFISHA AU KUUA SANAA ZA MAONYESHO HAPA NCHINI

Dhana ya sanaa imejadiliwa na wataalamu mbalimbali, baadhi ya wataalamu hao ni hawa wafuatao
Muhande P, and Balisidya (1976:1). Sanaa ni uzuri unajitokeza katika umbo lililosanifiwa, umbo ambalo mtu hulitumia kueleza hisia zinazomgusa kwa kutoa kielelezo au vielelezo vyenye dhana maalum. Wataalmu hawa wameainisha aina tatu za sanaa ambazo ni sanaa za uonyesho, sanaa za ghibu na sanaa za vitendo
Kwa mujibu wa Mhando na Balisidya (1976) wamekusanya mawazo ya wanazuaoni mbalimbali katika kufasili dhana ya sanaa za maonyesho. Mawazo makuu yaliyotolewa ni kama haya yafuatayo.

Kuna baadhi ya wataalam wanaodai kuwa sanaa za maonyesho ni michezo ya kuigiza au ni michezo ioneshwayo kwenye jukwaa lenye pazia na mataa mengi ya rangi au ni michezo ya Shakespeare kama vile “mabepari wa venisi”
Wengine wanadai kuwa sanaa za maonyesho ni vichekesho au ni maigizo yanayochekesha.
Pia sanaa za maonyesho huweza kufasiriwa kuwa ni maigizo.
Hivyo basi, Mhando na Balisidya (1976:2) wanasema kuwa, sanaa za maonyesho ni kitendo chochote chenye sifa nne ambazo ni  (i) michezo  (ii) mchezaji  (iii) uwanja wa kuchezea  na (iv) watazamaji, mfano wa karibu kudhihirisha nadharia hii ni tamthiliya (mchezo wa kuigiza) mfano: “wakati ukuta”.
Sanaa za maonyesho za asili yaani za jamii ambayo utamaduni wake ulikuwa haujaingiliwa na wakoloni (kigeni) kugawanywa katika makundi matano mbazo ni (i) sherehe (ii) ngoma (iii) masimulizi ya hadithi (iv) kusalia miungu (v) majigambo.
Kwa hiyo basi sanaa za maonyesho za Kiafrika ni dhana zilizo kwenye umbo linalotendeka na siyo mchezo. Ili dhana hii itendeke inahitajika mtu wa kutenda (mtendaji), mtendaji huyu anahitaji uwanja wa kutendea hiyo dhana na wakati akitenda hiyo dhana wanakuwepo watazamaji. Hivyo sanaa za maonyesho za Kiafrika ni kitendo chochote chenye sifa nne ambazo ni dhana inayotendeka, mtendaji, uwanja wa kutendea na watazamaji.
Ifuatayo ni hali ya sanaa za maonyesho kabla ya ukoloni hapa Afrika mashariki ni kwamba ilikuwa haijaingiliwa na utamaduni wa kigeni. Zifuatazo ni sanaa za maonyesho zilizokuwepo Afrika Mashariki.
SHEREHE
Sanaa za maonyesho katika kundi hili zinahusu kuingizwa kwa mwanajamii kwenye kundi la watu wa aina fualni kutoka kundi la watu wa aina nyingine kwa mfano jando na unyago. Mtu kutoka kundi la watoto kuingia kundi la watu wazima, au kutawazwa kwa chifu, kutoka kundi la raia na kuingia kundi la askari shujaa nk. Hivyo, kutoka kundi moja na kuingia kundi jingine ni hatua iliyopewa umuhimu mkubwa katika jamii ya asili.
NGOMA
Neno ngoma lina maana tatu yaani; “Ngoma” ni chombo cha muziki. “Ngoma” pia ni uchezeshaji wa viungo vya mwili wenye mtindo na miondoko  maalum pengine ukiambatana na muziki “Ngoma “ pia ni sherehe iwe ni jando, harusi, unyago nk. Hapa neno ngoma lina maana ya sherehe yoyote kwa ujumla na siyo lazima kwenye sherehe hiyo pawepo na ngoma uchezeshaji wa viungo au ngoma chombo cha muziki ingawaje mara nyingi katika hatua fulani ya sherehe hii kimojawapo huwepo.
Ngoma tunayoongelea katika sehemu hii ni ile yenye maana ya pili – uchezashaji wa viungo vya mwili wenye mtindo na miondoko maalum pengine ukiambatana na muziki.
Pia hapa tunaongelea ngoma ambazo haziamabatani na sherehe maalum mifano michache ni kama mpendo, msunyumbo (wagogo) silanga (wapogoro), Gombasugu (wazaramo), kitoto (wangoni) mtuya, ditonga (wakaguru) nk.
MASIMULIZI YA HADITHI
Tunazo hadithi za asili kwa maelfu kwani katika jamii ya asili masimulizi ya hadithi yalikuwa ni mojawapo ya mambo ya kila siku. Baada ya kazi nyingi za mchana wanajamii wakubwa kwa wadogo wake kwa waume, walikusanyika majumbani kwao na kujipumzisha kwa kusimuliana hadithi. Hadithi zote ziwe nikuhusu wanyama, ndege, bianadamu, mazimwi nk. Zina maana fulani ndani yake inayohusu maisha katika jamii, ubaya autendao mhusika katika hadithi kama vile ya “Mama wa kambo” na adhabu aipatayo huwa ni fundisho kwa wale wanaoisikiliza, hadithi kuepukana na ubaya huo katika kuishi na wenzao.
Mafunzo yatokanayo na hadithi yangaliweza kutolewa kwa maneno matupu lakini umuhimu wa mafunzo hayo ulisababisha yawekwe kwenye umbo la kisanaa ili yapate uzuri unaovutia wale wanaohusika. Sanaa hii pia ikiwa ya vitendo ili mafunzo yadhihilike zaidi mafano wa hadithi hizo ni “Mama wa Kambo”, “Mfalme aliyetaka Watoto wa Kike” “Kalukanga Mtoto  wa Nyoka nk.
Masimulizi ya hadithi mara nyingi huendeshwa ndani ya nyumba kuzunguka moto ambapo wasikilizaji hukaakumzunguka msimulizi wakati mwingine, hadi siku za mbalamwezi, masimulizi ya hadithi huweza kuwa nje ya nyumba. Vyovyote ilivyo  hapo wakaapo wasikizaji na masimulizi ndiyo uwanja wa kutendea
KUSALIA MIUNGU
Katika jamii ya asili watu walielekeza kwa miungu mbalimbali matatizo, ambayo wao kwa nguvu zao za kibinadamu yaliwashinda. Walipopata tatizo la ukame au waliposhambuliwa na magonjwa ya hatari, walipokabiliwa na manyama wala watu, walipokosa watoto nk. waliikabili miungu yao na kuisalia iwasaidie. Ufuatao ni mfano wa kusalia miungu unaotumika na wakagulu wakati wa kuomba mvua. Kusalia miungu huitwa Chijumba – Mulungu watu waki shaelekezwa na mganga kuwa ukame uliopo utamalizwa na Chijumba – Mulungu.
Katika mfano huu watendaji na uwanja wa kutendea ni dhahiri labda tutatatanishwa na watazamaji ambapo katika kusalia miungu watazamaji ni miungu wanaosalia kwa vile ndiyo inayotazama yale yanayotendeka
MAJIGAMBO
Majigambo ni masimulizi ya kujigamba kwa mtu kuhusu mambo ya kishujaa aliyopata kuyatenda maishani mwake. Majigambo haya husimuliwa katika lugha ya kishairi na masimulizi yake huambatana na vitendo vya mjigambaji mwenyewe. Kwa mfano, ikiwa anajigamba kuhusu vita fulani alivyopigana basi atatenda vitendo kuonesha vile alivyokwenda vitani, alivyokabiliana na adui, alivyomuua adui au adui alivyokimbia. Majigambo yanapatikana zaidi katika jamii za kanda ya ziwa magharibi hasa Wahaya na pia jamii za kusini mwa Tanzania kama Wahehe. Majigambo yalikuwa na madhumini ya kudumisha utu wa Wanaume katika jamii.
Sura ya sanaa za maonesho ilibadilika kutokana na kuja kwa wakoloni kutoka nchi za nje hasa Waingereza katika kuitawala Tanzania kuanzia baada ya vita vya kwanza vya dunia hadi Tanzania ilipopata uhuru mnamo mwaka 1961. Waingereza walisababisha mabadiliko mbalimbali katika sura nzima ya sanaa za maonyesho zifuatazo; ni mbinu zilizotumika kuua au kujifisha sanaa za maonyesho hapa nchini.
Waingereza walileta sanaa za maonyesho zenye asili ya utamaduni wa kwao hasa Drama. Drama ilingizwa hasa mashuleni ambapo waalimu wengi walikuwa Waingereza. Madhumuni ya kuingiza drama hayakuwa na uzito mkubwa. Waingereza hawa walikuwa wanatafuta kitu cha kupitisha muda wakati ambapo walikuwa hawana la kufanya.
Hivyo kutokana na kuingiza drama sanaa za maonyesho za Afrika zilikosa ushiriki, kwani wengi walihamasika kushiriki katika drama kwani walivutiwa zaidi katika uonyeshaji wenyewe mavazi ya washiriki, matumizi ya mataa za rangi nk.
Pia waingereza kuona drama ni bora zaidi kuliko sanaa za maonyesho za Kiafrika tamthilia zilizoongozwa ni zile zilizoandikwa na Waingereza zaidi zikiwa za yule mwanasanaa mashuhuri William Shakespeare. Baadhi ya kazi zilizovuma sana ni kama vile: Hamlet, Othello, Ceaser, Macbeth, Rumeo and Juliet na The Temped. Kwa upande wa Watanzania walioshiriki katika tamthilia walikuwa kama washiriki au watazamaji tu kwani, tamthilia hizi hazikuwa na maana yenye uzito wowote kwao kwani zilielezea utamaduni wa kigeni tu kitu. Hivyo sanaa zetu za maonesho hazikupata nafasi.
Mbinu nyingine walizotumia ni kutambulisha dini ya Kikristo. Kwa kutumia dini hii walifanya kila njia kukomesha mambo ambayo hasa yalikuwa sanaa za maonyesho za Kitanzania asilia kwa mfano; jando na unyago, kusalia miungu pamoja na ngoma. Mambo yote haya waliyaita ya kuwa ni ya kishenzi. Hivyo wakrito wote hawakupaswa kushiriki katika mambo hayo na pia walipaswa kuchukua jukumu la kukomesha mambo haya. Vilevile wale walioshiriki walionekana wanatenda dhambi. Hivyo basi kwa mbinu hii walifaulu kufifiza au kuua sanaa za maonyesho za Kiafrika.
Dhana ya kufananisha sanaa za maonesho na uchekeshaji, lilishika mizizi  barabara kwani hadi leo sanaa za maonesho zinaambatana na uchekeshaji, kama shughuli haichekeshi sio sanaa za maonyesho. Kwa hiyo kuna ugumu wa kumfanya mtazamaji mwenye mawazo haya kuelewa kuwa ngoma au unyago ni sanaa za maonesho.
Wazo hili la uchekeshaji pia limesababisha kudharauliwa kwa sanaa za maonesho. Watu wengi hawa kuona kuwa ni jambo la maana kwenda kutazama maonesho ambayo umuhimu wake ni kuchekesha. Basi ikawa sanaa za maonyesho ni shughuli ya watoto wadogo au labda watu wasiokuwa na kazi au wanaotafuta kuchekeshwa. Mawazo haya yameendea mpaka leo na ndiyo yaliyosababisha, kutokutiliwa mkazo kwa maendeleo ya sanaa za maonesho. Na hata vitabu vya tamthilia vilivyochapishwa mwanzo kwa lugha ya Kiswahili, Afrika mashariki vilikuwa na athari za vichekesho vitabu kama vile “Afadhali mchawi” “Mgeni karibu” “Nakupenda lakini”, “Nimelogwa nisiwe na Mpenzi” vilionekana havina umuhimu sana kwa jamii ya Afrika mashariki zaidi ya kuburudisha tu. Vitabu kama hivi vilisaidia kudumisha wazo la kudhani tamthilia ni vichekesho tu. Hivyo basi lilifisha au kuua sanaa za maonyeshao za kiafrika.
Uhusikaji wa Waafrika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Watu walitumia muda mwingi katika kuzalisha kwani, walichukuliwa wengi kwenda kufanya  kazi katika sekta mbalimbali za kiuchumi zilizoanzishwa na wageni, mfano; Waafrika wengi walichukuliwa kama manamba katika mashamba ya mkonge, hivyo basi kushindwa kushiriki kikamilifu katika suala la kuendeleza sanaa za maonyesho kitu ambacho kilisababisha sanaa za maonyesho kufifia kwa kiwango kikubwa kwani walikua wakilazimishwa kufanya kazi  hizo za kiuchumi.
Hivyo basi, katika kipindi cha ukoloni, sanaa za maonesho zilififia na kufa kutokana na mbinu zao za kukuza ukoloni. Aidha, katika kipindi hiki cha usasa, sanaa za maonesho zinazidi kufifia na kutoweka kutokana na mwingiliano wa jamii mbalimbali zenye tamaduni tofauti, mwendelezo wa shughuli za kikoloni kama elimu na dini pamoja na maendeleo ya sayansi na tekenolojia vinazidi kufifisha na kuua sanaa za maonesho za Kitanzania.

MAREJEO
Balisidya, M. L. (1987), “Tanzu na Fani za Fasihi Simulizi” katika Mulika nambari 19. Dar es Salaam: TUKI
Mhando, P na N. Balisidya (1976), Fasihi na sanaa za maonyesho; Tanzania Publishing HouseDar es salaam.    
Wamitila, K. W. (2004), Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Focus Publication: Nairobi Kenya.


No comments:

Post a Comment